Habari Mpya

Tuesday, 10 February 2015

GONO NI HATARI


Baada ya kufahamu namna ya kutibu gono, sasa tuangalie madhara ya ugonjwa huo. Moja ya madhara anayoweza kupata mtu kutokana na ugonjwa wa kisonono ni, mwanamke kutoweza kuzaa yaani kuwa mgumba au mimba kutoweza kutunga. Tunaelezwa kuwa magonjwa ya zinaa ya chlamydia na gono yana mchango katika kusababisha wanawake kutozaa kwani magonjwa hayo kwa asilimia 10 hadi 15 huweza kusababisha uvimbe katika fupanyonga au Pelvic Inflammatory Disease (PID) na hasa kwa kuwa wanawake wengi wenye kisonono huwa hawaonyeshi dalili. Ugonjwa wa PID husababisha makovu katika mirija ya uzazi hali ambayo husababisha kushika mimba kuwa kugumu na matatizo wakati wa ujauzito. PID ni ugonjwa unaopaswa kutibiwa haraka. Kwa upande wa wanaume ugonjwa wa kisonono pia huweza kuwafanya wanaume wasipate watoto kwani huwasababishia uvimbe katika sehemu ya mbele ya korodani ambako mbegu za kiume hutengenezwa. Uvimbe huo usipotibiwa husababisha utasa.

Ugonjwa wa gono pia huweza kuathiri moyo, ubongo, ngozi na kadhalika kwa hivyo ni hatari sana kwa mtu yoyote na unahitaji kutibiwa mapema. Pia ugonjwa huo huleta madhara au uvimbe kwenye maungio ya viungo, ambapo vimelea vinavyosababisha kisonono huweza kusambaa kwenye damu na kuleta maambukizo kwenye sehemu nyinginezo mwilini. Maambukizo hayo huleta homa, vipele, vidonda kwenye ngozi, maumivu ya viungo na uvimbe. Vilevile wanawake ambao ni wajawazito na wameambukizwa gono wako kwenye hatari ya mimba kutoka au kuzaa mapema kabla mimba haijatimiza umri wake (preterm labor). Kwa wale wanaoambukizwa gono kipindi cha kukaribia kujifungua, wanaweza kuwaambukiza watoto wao na hivyo watoto kupata ugonjwa wa uti wa mgongo (meningitis), kuwa vipofu, homa ya mapafu (pneumonia) na ugonjwa wa mifupa (septic arthritis).


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: GONO NI HATARI Description: Rating: 5 Reviewed By: Tatyana Celestine
Scroll to Top