Monday, 14 May 2018

MAMA KANUMBA ASEMA YAKE BAADA YA LULU KUTOKA GEREZANI


Siku mbili tangu alipoachiwa muigizaji Elizabeth Michael ’Lulu’, mama wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa amesema ameumia na tangu alipopata taarifa hizo hajalala.

Mama Kanumba amesema, tangu alipopata tetesi za msanii huyo ametoka jela, amejikuta anakosa usingizi na kuumwa presha.

Ameongeza na kusema, kutokana na suala hilo, imemlazimu jana Jumatatu kwenda kwenye maombi kwa ajili ya afya yake hiyo.

Amesema, licha ya kuwa si yeye aliyemuhukumu, Lulu alipaswa kukaa hata mwaka mmoja ili roho yake iridhike lakini ndio hivyo: "Siku zote maskini hana haki."

Hata hivyo,  amewashukuru wote waliohusika kumtoa na kuongeza kuwa yote ni kwa sababu yeye hana pesa na anajua watu wataanza kumtusi mitandaoni kwa sababu hiyo lakini yote anamuachia Mungu.

Jeshi la Magereza kupitia Ofisa Habari wake, Lucas Mboje, limesema Lulu amebadilishiwa adhabu na atatumikia kifungo cha nje kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment