Habari Mpya

Saturday 18 January 2014

Zanzibar kuweka Historia kupitia Fasheni


Wanamitindo walioshiriki kwenye onyesho la mitindo Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja. Picha na Salhim Shao 
Na Maimuna Kubegeya,Mwananchi


Tukio kubwa la mitindo kuwahi kutokea visiwani Zanzibar, ilikuwa  ni onyesho la mitindo la Fashion Night Out lililofanyika katika Mgahawa wa 6 Degree South, ndani ya viunga vya Ngome Kongwe.
Pamoja na kujulikana kama kitovu cha utalii, safari hii fasheni nayo iliingia kwenye rekodi kwa kuongezea sifa ya visiwa hivyo, pale watalii, wadau na wapenzi wa mitindo waliposhuhudia mitindo mipya iliyowakilishwa na mbunifu Doreen Mashika.
Shughuli ilianza kwa tafrija fupi ambayo ilitoa ukaribisho kwa wageni waalikwa kupata wasaa wa kujuana na kuzungumza mawili matatu, kabla mbunifu Doreen hajapanda jukwaani na kueleza dhamira yake ya kuwaleta pamoja wadau hao wa mitindo ndani  na nje ya nchi.
Onyesho lilianza mapema saa moja na nusu jioni, ambapo watu walikuwa wakipata kinywaji na vitafunwa maalumu, vilivyotengenezwa katika mahadhi ya kiitaliano.
Tofauti na maonyesho mengine onyesho hili lilikuwa na steji ndogo kuliko  ilivyozoeleka. Si hivyo tu hata mtindo uliotumika kuwakilisha kazi hizo za ubunifu ulikuwa ni wa kipekee wenye utofauti mkubwa.
Kulikuwa na wanamitindo watano ambapo kila mmoja alionyesha umahiri wake katika kulitawala jukwaa. Wote walikuja na mavazi ya kisasa wakiwa na mitindo rahisi ya nywele.
Wanamitindo waliingia na kutoka wakionyesha mavazi mbalimbali ya wanawake. Magauni marefu na mafupi pamoja na jumpsuit yalitawala onyesho hilo.
Kwa upande wa mitindo ya nywele warembo hao walipambwa kwa maweaving, rasta za kawaida pamoja na mawigi huku mapambo yao yakikamilishwa na  ‘make’ up ya aina yake.
Wanamitindo waliokuwepo katika onyesho hilo ni  Suzane Manoko, Joselyne Mrashi na Anna Gura  wote kutoka Tanzania na Dianne Nyanzwa na Suzanne Anyango kutoka Kenya
Kila mmoja alionyesha umahiri wake katika kunadi vazi alilovaa, vilevile kuonyesha uhusiano ulioko kati ya urembo na  mapambo yaliyotumika kunakshi mitindo yao.
Mbunifu Doreen Mashika alikuwa na kazi moja tu ya kuonyesha kipaji alichonacho katika ubunifu wa mitindo. Hivyo alipata wasaa wa kuwapamba wanamitindo wake kwa kutumia mapambo ya kiafrika yaliyotengenezwa kwa mikono.
Mashika hakusita kuelezea sababu hasa inayotofautisha kazi zake na watu wengine pale alipobainisha kuwa asilimia kubwa ya kazi zake hizo ni za mikono. Na ni za kitanzania halisi. Wakati anaingia jukwaani Mashika aliingia na mtaalamu wa vipodozi na urembo kutoka nchini Afrika Kusini, Swiss Reto Camichel  aliyekuwa na kazi moja tu ya kuwabadilisha mitindo ya nywele wanamitindo waliokuwa jukwaani hapo.

Kwa mbwembwe mtaalamu huyo aliingia na ‘trei’ ndogo mkononi yenye kitana, ‘spray’ ya nywele na brashi ya kujipodolea, hivyo ndivyo vilikuwa vifaa vyake vya kazi.
Baadaye ilikuwa ni mwendo wa kupishana stejini, wakati Doreen akimwekea mwanamitindo mapambo, Camichel alikuwa na kazi moja tu ya kurekebisha ‘make up’ na kuboresha muonekano wa nywele.
Wakati akiendelea na kazi zake hizo,  hakusita kueleza dhamira kubwa iliyomleta kwenye mgahawa ule. Kwani alibainisha kuwa atakachokifanya pale ni kuonyesha uhusiano uliopo kati ya mavazi  na vipodozi kwa ujumla. Inavutia kuona nguo uliovaa inaendana siyo tu na vipodozi bali hata na mtindo wako wa nywele.
Maimuna Kubegeya
Kwa muda wote wataalamu hao walikuwa wakionyesha umahiri wako katika kuwapamba na kuwavalisha wanamitindo waliokuwa stejini aina mbalimbali za uvaaji huku wakiburudishwa na muziki laini.
Mastaa mbalimbali walikujumuika pamoja na wadau na wapenzi wa mitindo kuangalia yanayojiri ndani ya usiku huo wa mitindo.
Wabunifu Ally Remtulah, Vida Mahimbo, Lucky Roberto, Martin Kadinda na wengine kibao walikuwepo mgahawani hapo kumpa sapoti mbunifu mwenzao Doreen Mashika.
Fashion Night Out ilikuwa ni onyesho la aina hiyo kuwahi kufanyika visiwani Zanzibar, ambapo waandaaji wake waliahidi kuendelea kulifanya kila mwaka.
Katika onyesho hilo mbunifu Doreen Mashika alikuwa akionyesha toleo lake la 19, tangu aanze kazi za ubunifu wa mitindo mwaka 2006.
Doreen ni miongoni mwa wanamitindo wa kitanzania waliowahi kufanya maonyesho ya kazi zao nje ya nchi.
Baadhi ya nchi alizowahi kufanya maonyesho ni  Ufaransa, Ujerumani, Kenya, Ethiopia  na Afrika Kusini.
Fashion Night Out ni onyesho la kwanza kuwahi kufanyika nchini chini ya uandaaji wake mbunifu Doreen Mashika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: Zanzibar kuweka Historia kupitia Fasheni Description: Rating: 5 Reviewed By: fashion time na tatyana celestine
Scroll to Top