Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye anatarajiwa
kuwa mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Mashindano ya Miss Tanzania mwaka
2016 yatakayofanyika Machi 19, 2016 jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia
mashindano hayo leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Lino
International Agency Limited kampuni inayoandaa mashindano hayo Bw.
Hashim Lundenga amesema kuwa uzinduzi huo kwa mwaka 2016 utakuwa wa aina
yake tofauti na miaka iliyopita.
“Tunatarajia
kutangaza kamati mpya ya Miss Tanzania siku hiyo ya uzinduzi, kamati ya
Miss Tanzania itakuwa na jukumu la kuusaidia uongozi wa Miss Tanzania
katika shughuli nzima za kuratibu na kusimamia mashindano hayo.” alisema Lundenga.
Lundenga
ameongeza kuwa, katika uzinduzi huo wadau mbalimbali wa tasnia ya
urembo wakiwemo wabunifu wa mavazi, mawakala wanaoandaa mashindano ya
Miss Tanzania katika ngazi mbalimbali hapa nchini watakutana .
Aidha
amesema uzinduzi wa Miss Tanzania mwaka 2016 umedhaminiwa na makampuni
ya Ramada Resorts Dar, Naf Beach Hotel Mtwara, Kitwe General Trader, CXC
Africa, MMI Tanzania, Mwandago Invesment Ltd, Break Point na GSM Media.
Vilevile
uzinduzi huo utahamia mkoa wa Arusha mara tu baada ya kufanyika mkoa
wa Dar es Salaam. Wasanii Linah Sanga anayeimba nyimbo za kizazi kipya
na Wanne Star msanii wa ngoma za asili watatoa burudani katika uzinduzi
huo.
Mashindano
ya Miss Tanzania yalifungiwa kwa miaka miwili mfululizo na Baraza la
Sanaa Tanzania (BASATA) Desemba 22, 2014 kutokana na kukiuka Sheria,
Kanuni na Taratibu za uendeshaji matukio ya Sanaa nchini,
kutokuwasilisha nyaraka mbalimbali za shindano lake hususan mikataba ya
washiriki pamoja na kutumia mawakala wasiosajiliwa na kupewa vibali vya
BASATA.
Mashindano
hayo yamefunguliwa tena na BASATA Agosti, 2015 baada ya mwandaaji wake
LINO International Agency Limited kufuata taratibu ikiwemo kuomba radhi
na kuyafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza pamoja na
kutekeleza masharti aliyopewa.
0 comments:
Post a Comment