Dar es Salaam/ Arusha.
Kashfa ya aliyekuwa Miss Tanzania, Sitti Mtemvu imechukua sura mpya
baada ya Wakala wa Uzazi, Vifo na Ufilisi (Rita) kusema kuwa
wamekamilisha upekuzi wa taarifa alizotumia kuombea cheti cha kuzaliwa
na vielelezo hivyo vimelekwa polisi vikafanyiwe kazi.
Wakizungumza
na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, Ofisa mtendaji mkuu wa Rita,
Phillip Saliboko na Meneja masoko na mawasiliano, Josephat Kimaro
walisema upekuzi wa nyaraka zilizotumiwa na Sitti uliofanywa na
wanasheria wao, tayari umekamilika.
“ na kinachofuatasasa n i kupeleka nyaraka hizo kwenye mamlaka inayohusika ambayo ni polisi, wao ndio wataamua nini cha kufanya,” alisema Kimaro.
Alisema
Rita haiwezi kumhukumu moja kwa moja mrembo huyo kuwa alighushi nyaraka
na kudanganya ili apate cheti hicho cha kuzaliwa kilichotolewa na Rita
Septemba na badala yake wanapeleka vielelezo walivyonavyo polisi ili nao
wavifanyie kazi.
“Sisi (Rita) jukumu letu lilikuwa ni
upekuzi wa nyaraka, kazi ambayo imefanywa kwa ustadi mkubwa na jopo la
wanasheria wetu na hadi sasa imekamilika na kinachofuata ni kuzipeleka
nyaraka hizo polisi ambao wao ndiyo wenye jukumu la uchunguzi na
kumchukulia hatua Sitti au la,” alisema.
“Tukibaini mtu ametumia udanganyifu ili kupata cheti,
kwanza huwa tunamfutia cheti chake na taratibu nyingine za kisheria
zinafuata. Tunafanya hivyo kwa watu wote wanaokuja kuomba vyeti kwetu na
siyo kwa Miss Tanzania peke yake japo hili la Sitti tunaiachia mamlaka
husika ifanye kazi yake,” alisema.
Sitti Mtemvu
aliingia kwenye kashfa ya kudanganya umri wake na nyaraka zake
mbalimbali zilionyesha alizaliwa 1989, umri ambao umepitiliza ule
unaotakiwa kwa mshiriki wa mashindano ya Miss Tanzania, huku cheti chake
kikionyesha alizaliwa 1991, hivyo kulazimika kuvua taji hilo.
Wakati
huohuo, mrembo aliyevikwa taji la Miss Tanzania nambari mbili, Lilian
Kamazima anatarajiwa kuwasili leo mjini Arusha na kupokewa kwa shangwe
akiwa na taji lake.
Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi
wa Kampuni ya Mwandago Entertainment Ltd, Faustine Mwandago iliyosimamia
ushindi wake ngazi ya kanda ilisema kuwa mrembo huyo atawasili kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) saa 6:00 mchana.
Mwandago
alisema kuwa mrembo huyo atapokelewa na wenyeji wake, wakiwamo wazazi
wake na kisha kupanda gari la wazi ili kuwapa fursa wakazi wa Arusha
kumshuhudia.
Alisema kuwa mara baada ya kuwasili Arusha
atapelekwa moja kwa moja nyumbani kwao, Sakina ili kushiriki hafla
aliyoandaliwa na wazazi wake pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.
Wakazi
wa Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi kumpokea mrembo huyo kwa
lengo la kumpa moyo na kulikaribisha taji hilo mara baada ya ukame wa
muda mrefu wa kupata taji la Miss Tanzania.
Imani Makongoro na Moses Mashalla, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment