Na Maimuna Kubegeya,Mwananchi
Tukio kubwa la mitindo kuwahi kutokea visiwani
Zanzibar, ilikuwa ni onyesho la mitindo la Fashion Night Out
lililofanyika katika Mgahawa wa 6 Degree South, ndani ya viunga vya
Ngome Kongwe.
Pamoja na kujulikana kama kitovu cha utalii,
safari hii fasheni nayo iliingia kwenye rekodi kwa kuongezea sifa ya
visiwa hivyo, pale watalii, wadau na wapenzi wa mitindo waliposhuhudia
mitindo mipya iliyowakilishwa na mbunifu Doreen Mashika.
Shughuli ilianza kwa tafrija fupi ambayo ilitoa
ukaribisho kwa wageni waalikwa kupata wasaa wa kujuana na kuzungumza
mawili matatu, kabla mbunifu Doreen hajapanda jukwaani na kueleza
dhamira yake ya kuwaleta pamoja wadau hao wa mitindo ndani na nje ya
nchi.
Onyesho lilianza mapema saa moja na nusu jioni,
ambapo watu walikuwa wakipata kinywaji na vitafunwa maalumu,
vilivyotengenezwa katika mahadhi ya kiitaliano.
Tofauti na maonyesho mengine onyesho hili lilikuwa
na steji ndogo kuliko ilivyozoeleka. Si hivyo tu hata mtindo
uliotumika kuwakilisha kazi hizo za ubunifu ulikuwa ni wa kipekee wenye
utofauti mkubwa.
Kulikuwa na wanamitindo watano ambapo kila mmoja
alionyesha umahiri wake katika kulitawala jukwaa. Wote walikuja na
mavazi ya kisasa wakiwa na mitindo rahisi ya nywele.
Wanamitindo waliingia na kutoka wakionyesha mavazi
mbalimbali ya wanawake. Magauni marefu na mafupi pamoja na jumpsuit
yalitawala onyesho hilo.
Kwa upande wa mitindo ya nywele warembo hao
walipambwa kwa maweaving, rasta za kawaida pamoja na mawigi huku mapambo
yao yakikamilishwa na ‘make’ up ya aina yake.
Wanamitindo waliokuwepo katika onyesho hilo ni
Suzane Manoko, Joselyne Mrashi na Anna Gura wote kutoka Tanzania na
Dianne Nyanzwa na Suzanne Anyango kutoka Kenya
Kila mmoja alionyesha umahiri wake katika kunadi
vazi alilovaa, vilevile kuonyesha uhusiano ulioko kati ya urembo na
mapambo yaliyotumika kunakshi mitindo yao.
Mbunifu Doreen Mashika alikuwa na kazi moja tu ya
kuonyesha kipaji alichonacho katika ubunifu wa mitindo. Hivyo alipata
wasaa wa kuwapamba wanamitindo wake kwa kutumia mapambo ya kiafrika
yaliyotengenezwa kwa mikono.
Mashika hakusita kuelezea sababu hasa
inayotofautisha kazi zake na watu wengine pale alipobainisha kuwa
asilimia kubwa ya kazi zake hizo ni za mikono. Na ni za kitanzania
halisi. Wakati anaingia jukwaani Mashika aliingia na mtaalamu wa
vipodozi na urembo kutoka nchini Afrika Kusini, Swiss Reto Camichel
aliyekuwa na kazi moja tu ya kuwabadilisha mitindo ya nywele wanamitindo
waliokuwa jukwaani hapo.
Kwa mbwembwe mtaalamu huyo aliingia na ‘trei’ ndogo mkononi
yenye kitana, ‘spray’ ya nywele na brashi ya kujipodolea, hivyo ndivyo
vilikuwa vifaa vyake vya kazi.
Baadaye ilikuwa ni mwendo wa kupishana stejini,
wakati Doreen akimwekea mwanamitindo mapambo, Camichel alikuwa na kazi
moja tu ya kurekebisha ‘make up’ na kuboresha muonekano wa nywele.
Wakati akiendelea na kazi zake hizo, hakusita
kueleza dhamira kubwa iliyomleta kwenye mgahawa ule. Kwani alibainisha
kuwa atakachokifanya pale ni kuonyesha uhusiano uliopo kati ya mavazi
na vipodozi kwa ujumla. Inavutia kuona nguo uliovaa inaendana siyo tu na
vipodozi bali hata na mtindo wako wa nywele.
Maimuna Kubegeya
Kwa muda wote wataalamu hao walikuwa wakionyesha
umahiri wako katika kuwapamba na kuwavalisha wanamitindo waliokuwa
stejini aina mbalimbali za uvaaji huku wakiburudishwa na muziki laini.
Mastaa mbalimbali walikujumuika pamoja na wadau na wapenzi wa mitindo kuangalia yanayojiri ndani ya usiku huo wa mitindo.
Wabunifu Ally Remtulah, Vida Mahimbo, Lucky
Roberto, Martin Kadinda na wengine kibao walikuwepo mgahawani hapo kumpa
sapoti mbunifu mwenzao Doreen Mashika.
Fashion Night Out ilikuwa ni onyesho la aina hiyo
kuwahi kufanyika visiwani Zanzibar, ambapo waandaaji wake waliahidi
kuendelea kulifanya kila mwaka.
Katika onyesho hilo mbunifu Doreen Mashika alikuwa
akionyesha toleo lake la 19, tangu aanze kazi za ubunifu wa mitindo
mwaka 2006.
Doreen ni miongoni mwa wanamitindo wa kitanzania waliowahi kufanya maonyesho ya kazi zao nje ya nchi.
Baadhi ya nchi alizowahi kufanya maonyesho ni Ufaransa, Ujerumani, Kenya, Ethiopia na Afrika Kusini.
Fashion Night Out ni onyesho la kwanza kuwahi kufanyika nchini chini ya uandaaji wake mbunifu Doreen Mashika.
No comments:
Post a Comment