Habari Mpya

Monday, 28 October 2013

ZIJUE PIA ONA MAHALA PANAPOFAA,ZINGATIA WAKATI.

TAFITI za kisayansi zimebaini kuwa nguo za ndani hasa zinazobana kwa wanaume na zile za aina ya nailoni (nylon) zinaathiri uwezo wa mbegu za kiume, hivyo kushindwa kutunga mimba.

Utafiti huo uliofanyika katika nchi za Ufaransa na Uingereza na kuchapishwa katika Gazeti la Daily Mail la Uingereza unabainisha kuwa, wanaume wanaovaa nguo za ndani zinazobana na zile zilizotengezwa kwa malighafi ya nailoni, mbegu zao za kiume (manii) huwa nyepesi na kupoteza uwezo wa kutunga mimba.

Vazi la ndani la wanaume linalojulikana kama boksa na nguo nyingine za ndani za kubana zenye asili ya nailoni, zinakuwa na athari kubwa zaidi hasa zinapovaliwa katika sehemu zenye joto, kama Dar es Salaam.

Kutokana na matokeo hayo, wanasayansi wameonya kuwa wanaume wanapaswa kuchukua tahadhari, hasa kutokana na tafiti nyingi za karibuni kuthibitisha kuongezeka kwa matatizo ya mbegu za kukosa uwezo wa kutunga ujauzito katika nyumba ya uzazi ya mwanamke.
Akizungumzia utafiti huo jana, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika Hosipitali ya Taifa Muhimbili, Dk Cyril Massawe, alisema una ukweli kutokana na mbegu za kiume kuwa nje ya mwili wa mwanamume tofauti na mwanamke ambaye kizazi chake kipo ndani.

“Kwa kawaida mwanamume anayeishi maeneo ya joto anapaswa kuwa makini sana, ili kuhifadhi vizuri manii yake anatakiwa kutumia mavazi yenye kupitisha hewa,” alisema Dk Massawe.

Ufaransa na Uingereza
Utafiti uliofanywa Ufaransa umebaini kuwa, upungufu wa nguvu za kiume kwa wanaume wengi ulianza kutokea tangu mwanzoni mwa 1990.

Awali, ilikuwa ikiaminika kuwa kupungua kwa uwezo wa mbegu za kiume kulitokana na sababu kama vile mtindo wa maisha, ulaji na matumizi ya dawa kupindukia na matumizi ya vyakula vyenye kemikali nyingi, lakini safari hii utafiti umebaini kuwa matumizi ya nguo za ndani yamekuwa yakiwaathiri wanaume wengi.

Mtafiti wa Uingereza, Profesa Richard Sharpe anasema tatizo hilo linaweza kuepukwa ikiwa mhusika atajitahidi kuvaa nguo zinazokubalika na mahala alipo. Hata hivyo, anapendekeza uchunguzi zaidi ufanywe ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho.

Mtafiti huyo kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh anasema: “Uingereza suala hili halijawahi kuonekana wala kutiliwa mkazo na kuwa kipaumbele katika afya, labda kwa sababu ya wasiwasi kwamba sehemu za mwanamume zinatakiwa kubanwa. Hivi sasa hakuna shaka kwamba suala hilo ambalo liliongelewa hapo awali lina ukweli ndani yake, hivyo ni wakati kwa watu wote kuchukua hatua.”

“Kutokuchukua hatua kutasababisha familia nyingi kukosa watoto na hivyo idadi ya watu itapungua, lakini katika hali ya kawaida, ni vyema watu wakaelimishwa namna ya uvaaji. Sehemu za joto mtu anatakiwa kuvaa pamba na si nailoni ili kulinda mbegu zake.”

Profesa Sharpe anasema bado wanasayansi wana kazi kubwa kwani mpaka sasa karibu kila eneo ambalo wanasayanasi wamelichunguza limebainisha kuchangia tatizo hilo, lakini mpaka sasa wanafikiri kuwa vyakula vyenye mafuta na vile vyenye kemikali nyingi vina mchango mkubwa zaidi katika tatizo hilo.

Watafiti ambao walitumia takwimu kutoka katika vituo vya afya 126, waligundua kuwa tangu mwaka 1989 mpaka 2005, kulikuwa upungufu wa uwezo wa manii kwa mwanamume kufanya kazi kwa asilimia 32.2, kiwango ambacho ni karibu asilimia mbili kwa mwaka.

Watafiti walisema: “Kwa ufahamu wetu, ni utafiti wa kwanza kufanyika na umehusisha mbegu za kiume hai na uwezo wa manii katika nchi nzima kwa kipindi kirefu.”
“Huu ni utafiti mkubwa na unatoa onyo kali kiafya kwa jamii. Lakini huwezi kumlazimisha mtu kuhusu matumizi ya nguo za ndani,” wanasema.

kwa msaada wa  gazeti la mwananchi
Posted  Ijumaa,Decemba7  2012  saa 23:58 PM.


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: ZIJUE PIA ONA MAHALA PANAPOFAA,ZINGATIA WAKATI. Description: Rating: 5 Reviewed By: fashion time na tatyana celestine
Scroll to Top